Elizabeth Itaja
Utafiti huu umechunguza athari za kimofolojia za lugha ya Kihehe katika ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya pili kwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani Kilolo, mkoani Iringa. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Uhawilishaji Lugha ya Lado (1957), inayosisitiza kuwa lugha ya kwanza (L1) huathiri ujifunzaji wa lugha ya pili (L2). Malengo ya utafiti yalikuwa kubainisha vipengele vya kimofolojia vya Kihehe vinavyotofautiana na Kiswahili, kueleza athari zake katika ujifunzaji wa Kiswahili, pamoja na kubainisha mbinu bora za ufundishaji zinazoweza kupunguza athari hizo. Utafiti umetumia mkabala wa kimaelezo, na data zilikusanywa kwa kutumia ushuhudiaji na mahojiano. Sampuli ya utafiti ilihusisha washiriki 76, wakiwemo wanafunzi 60 na walimu wa Kiswahili 16 kutoka shule nne za msingi. Uchambuzi wa data ulifanyika kwa kutumia uchanganuzi linganishi, uchambuzi wa makosa na uchanganuzi wa kimaudhui. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa lugha ya Kihehe inaathiri kwa kiasi kikubwa matumizi ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, hususan katika vipengele vya viambishi vya nafsi, viyeyusho /w/ na /y/, uchopekaji wa irabu /i/ na /u/, uchopekaji wa konsonanti /h/, pamoja na matumizi ya viambishi vya ukubwa na udogoshi. Athari hizi husababisha makosa ya kimofolojia yanayoathiri ufasaha wa Kiswahili sanifu na wakati mwingine kupotosha maana. Aidha, utafiti ulibaini kuwa mbinu bora za kupunguza athari hizo ni pamoja na matumizi ya mbinu shirikishi na tendaji, mazoezi ya kuzungumza na kuandika, pamoja na mrejesho wa mara kwa mara kwa wanafunzi. Utafiti unapendekeza serikali na watunga mitaala kuimarisha ufundishaji wa Kiswahili katika mazingira ya wingilugha kwa kutoa mafunzo ya walimu na nyenzo zinazozingatia changamoto za lugha ya kwanza. Kwa ujumla, utafiti huu umeonesha kuwa athari za Kihehe katika ujifunzaji wa Kiswahili ni dhahiri na zinathibitisha kuwa lugha ya kwanza ina nafasi kubwa katika ujifunzaji wa lugha ya pili, hivyo kuna umuhimu wa kutumia mikakati ya ufundishaji inayozingatia muktadha wa kiisimu wa mwanafunzi.