Everlyne Riimi Njagi, John Khaisie Wanyama, Timothy Kinoti M’Ngaruthi
Muziki ni mojawapo ya maeneo muhimu zaidi ya kuchunguza namna lugha hujenga fikra za kijinsia katika jamii. Utafiti huu unachunguza sifa za mwanamke zinazotokana na matumizi ya sitiari katika nyimbo tano teule za Newton Kariuki Ndwiga, anayejulikana kwa jina la kisanaa la Newton Karish. Makala hii imechunguza sifa za mwanamke zinazodhihirika kupitia kauli za kisitiari katika nyimbo za msanii huyu. Kwa kuongozwa na Nadharia ya Sitiari za Kidhana ya Lakoff na Johnson (1980), utafiti huu umechukulia sitiari sio tu kama pambo la lugha bali kifaa cha kiakili na kijamii kinachotumiwa na jamii kumfafanua, kumthamini, kumkosoa au kumdhibiti mwanamke. Utafiti ulikuwa wa kithamano. Nyimbo tano zenye matumizi mengi ya sitiari ziliteuliwa kimakusudi na kuchanganuliwa kwa mbinu ya uchanganuzi wa matini. Matokeo yanaonyesha kuwa msanii anamsawiri mwanamke kama mwenye bidii, akili, ushindani, uwezo wa kuongoza na uwezo wa kubadili mwelekeo wa uchumi wa familia. Hata hivyo, sitiari nyingine zinamsawiri kama asiye mwaminifu, mwenye kubadilikabadilika, mwenye kelele, mwenye majivuno, mwenye tamaa, hatari kwa jamii na anayewaathiri wanaume na familia kwa jumla kihisia. Utafiti huu umehitimisha kuwa sitiari katika nyimbo hizi zinafanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Kwa upande mmoja, zinapongeza uwezo wa mwanamke katika elimu na maendeleo ya familia. Kwa upande mwingine, zinaendeleza hofu za kijamii kuhusu uhuru wa mwanamke, harakati zake, na mamlaka yake. Kitaaluma, makala hii inachangia kuelewa jinsi sitiari katika fasihi simulizi zinavyoshiriki katika kujenga maana za kijinsia na taswira zinazokinzana kuhusu mwanamke.